WHO INACHUNGUZA UGOJWA MPYA UNAOUA WATU SUDAN KUSINI


Shirika la afya duniani (WHO) linasema kuwa linachunguza vifo vya watu wapatao 100 waliokufa kwa ugonjwa ambao bado haujajulikana katka eneo la Fangak, lililopo katika jimbo la Jonglei, katika Sudan Kusini.

Wiki iliyopita, wizara ya afya ya nchi hiyo iliripoti kuwa ugonjwa usiojulikana umewauwa mamia ya watu katika eneo hilo ambalo pia lilipatwa na mafuriko makubwa.

Afisa wa afya katika eneo hilo amesema kuwa sampuli za awali zilizokusanywa kutoka katika eneo hilo zilionyesha matokeo hasi ya kipindupindu.

"Tumeamua kutuma ujumbe wa dharura kwenda huko na kufanya tathmini ya hatari na kuchunguza; hapo ndipo tutakapoweza kukusanya sampuli kutoka kwa watu– lakini idadi ya awali tuliyoipata ni kwamba kulikuwa na vifo ,” amesema Bi Sheila Baya.

Amesema kuwa eneo la Fangak haliwezi kufikiwa kwa njia ya barabara kutokana na mafuriko na ujumbe wa WHO ulikuwa unasubiri helikopta iwarudishe katika mji mkuu Juba, siku ya Jumatano.

Previous Post Next Post