Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali za nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki zitaendelea kuchukua hatua za makusudi za kukuza michezo ndani ya jumuiya hiyo.
Amesema kuwa hivi sasa, sekta ya michezo imekuwa chanzo kikubwa cha biashara, utalii, kuimarisha afya na ajira kwa vijana.
Amesema hayo leo (Jumatatu, Desemba 06, 2021) wakati wa akifungua mashindano ya 11 ya Mabunge ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Jijini Arusha.
“Nitoe wito tuendelee kutumia majukwaa ya namna hii kwa lengo la kubadilishana mawazo kuhusu namna bora ya kuimarisha ushirikiano wetu kwa ajili ya mustakabali na manufaa makubwa ya wananchi wetu”
Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa michezo hiyo lengo lake kuu ni kuimarisha mahusiano na kuifanya jumuiya ya Afrika Mashariki kuwa imara zaidi “Majukwaa ya namna hii yamekuwa chachu ya kuleta mwamko mkubwa wa masuala ya sanaa, burudani na michezo ndani ya jumuiya”
Pia, Waziri Mkuu amewasihi wabunge hao waendelee kuimarisha ushiriki wao kwenye masuala ya michezo kwani imekuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha afya na hivyo kusaidia kupambana na magonjwa yasiyoambukiza. “Kwa hiyo, nitoe rai kwa Bunge la Afrika Mashariki kusimamia kwa karibu ushiriki wa michezo kwa wabunge na hata wananchi wa Jumuiya yetu”
Kaulimbiu ya Mashindano hayo ni “Strengthening Integration through Inter-Parliamentary Games in the Covid-19 era" yaani kuimarisha masuala ya mtangamano katika kipindi hiki cha UVIKO-19 kupitia Mashindano ya Mabunge ya Jumuiya.


