SERIKALI KUENDELEA KUKUZA THAMANI YA MAZAO NA BIDHAA KUFIKIA DIRA YA TAIFA 2050





Na Mwandishi wetu Dodoma 

 Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dennis Londo, amesema Serikali kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuongeza thamani ya mazao na kuimarisha uzalishaji wa bidhaa, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.


Mhe. Londo amesema hayo leo, Agosti 7, 2026, baada ya kutembelea mabanda ya taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo katika Maonesho ya Kitaifa ya Nanenane yanayoendelea jijini Dodoma. Taasisi alizotembelea ni pamoja na Wakala wa Vipimo (WMA), Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) pamoja na taasisi nyingine zinazoshiriki katika maonesho hayo.


Amesema sekta za kilimo, mifugo na uvuvi zina mchango mkubwa katika maendeleo ya viwanda kwa kuwa mazao yake hutumika kama malighafi na pia huingia moja kwa moja kwenye masoko ya ndani na nje ya nchi. Hivyo, taasisi zilizo chini ya Wizara zina jukumu muhimu la kuhakikisha mazingira bora ya biashara na uzalishaji yanaendelea kuimarishwa.


“Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameelekeza kuwa tuendelee kutengeneza mazingira rafiki kwa Watanzania, iwe ni mkulima, mfugaji au mvuvi, kwa kupunguza gharama za uzalishaji. Gharama hizo zikishuka, wananchi wataongeza tija na faida katika shughuli zao,” amesema Mhe. Londo.


Ameeleza kuwa Serikali imeendelea kuwekeza katika miundombinu muhimu ikiwemo barabara, madaraja na vivuko vinavyorahisisha usafirishaji wa mazao kutoka maeneo ya uzalishaji kwenda viwandani na masokoni.


Aidha, amesema upanuzi wa huduma za umeme kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) umeendelea kufikisha nishati katika vijiji na vitongoji, hatua inayochochea uzalishaji wa viwandani na kupunguza gharama za uzalishaji kwa wananchi.


Maonesho ya Kitaifa ya Nanenane yanaendelea jijini Dodoma na leo yamefikia siku ya saba tangu kuanza kwake, huku kilele chake kikitarajiwa kufanyika kesho, Agosti 8, 2026, ambapo Mgeni Rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Previous Post Next Post