CRDB YAFANYA MAGEUZI MAKUBWA YA MFUMO WA KIBENKI, YAONGOZA MAPINDUZI YA KIDIGITALI

 




Na Lilian Ekonga.......

Benki ya CRDB imefanikiwa kukamilisha mageuzi makubwa ya mfumo wake mkuu wa kibenki, hatua ambayo imeleta mabadiliko chanya katika sekta ya fedha nchini. Mageuzi haya yameimarisha usalama wa miamala, kuongeza ufanisi wa utoaji huduma, na kuwezesha upanuzi wa huduma za kifedha ndani na nje ya Tanzania.


Kwa kutumia teknolojia ya kisasa, ikiwemo akili mnemba (AI), CRDB imeongeza kasi ya kutoa huduma kwa wateja, kupunguza hitilafu za kiufundi, na kutengeneza mazingira bora kwa huduma bunifu. Mageuzi hayo pia yameiwezesha benki hiyo kuimarisha uwepo wake katika nchi jirani kama Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), huku ikiwa imejiandaa kupanua huduma zake hadi Mashariki ya Kati na Ulaya.


Mafanikio haya yamepongezwa na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT), Emmanuel Tutuba, ambaye amesema mageuzi hayo ni ya kimkakati na yanadhihirisha ukomavu wa sekta ya fedha nchini. “CRDB imeonyesha uongozi wa mfano katika kusimamia mabadiliko makubwa ya kidijitali bila kuathiri huduma kwa wateja,” alisema.


Akizungumza na waandishi wa habari katika Makao Makuu ya CRDB jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Benki hiyo na Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, Bi. Tully Esther Mwambapa, alisema:




“Hakuna safari ya mageuzi isiyo na changamoto. Katika kipindi cha mabadiliko, baadhi ya wateja walikumbana na hitilafu za muda, lakini timu yetu ya wataalamu imekuwa ikifanya kazi kwa bidii kurejesha huduma katika hali ya kawaida. Leo hii tunajivunia kuwa na mfumo imara unaowezesha huduma bora ndani na nje ya Tanzania.”


Ubunifu wa CRDB umefungua milango ya ushirikiano wa kimataifa, ikiwemo makubaliano na kampuni ya Huawei kwenye mageuzi ya kidijitali, na mashirikiano na Crop Trust katika kukuza usalama wa chakula kupitia kilimo stahimilivu. Hili limezidi kuifanya Tanzania kuwa kivutio cha uwekezaji wa kifedha na teknolojia barani Afrika.


Viongozi wa serikali na sekta binafsi pia wamepongeza hatua hiyo, wakisema kuwa mageuzi ya CRDB ni ushahidi wa uwezo wa taasisi za kifedha za ndani kuhimili ushindani wa kimataifa na kuchochea ukuaji wa uchumi






.

Previous Post Next Post