Na Humphrey Msechu, Geita
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa, ametembelea banda la Benki Kuu ya Tanzania (BoT) katika Maonesho ya Tano ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea mjini Geita, ambapo alipatiwa maelezo ya kina kuhusu namna BoT inavyonunua dhahabu kutoka kwa wachimbaji wa ndani ili kuongeza akiba ya fedha za kigeni na kuimarisha uchumi wa taifa.
Akitoa elimu kwa wananchi na viongozi waliotembelea banda hilo, Afisa wa Idara ya Masoko ya Fedha BoT, Bi. Rehema Kassim, alisema kuwa ununuzi wa dhahabu ni mojawapo ya mikakati ya Benki Kuu katika kuhifadhi thamani ya fedha na kuongeza akiba ya fedha za kigeni. Alieleza kuwa tangu Oktoba 2023, BoT imeanza rasmi kutekeleza mpango wa kununua dhahabu moja kwa moja kutoka kwa wachimbaji wakubwa na wadogo kwa bei ya ushindani ya kimataifa.
Mpango huo umewekewa msingi wa kisheria kupitia kifungu cha 59 cha Sheria ya Madini, ambacho kinamtaka kila mchimbaji kuuza angalau asilimia 20 ya dhahabu yake kwa BoT. Ili kuleta mvuto zaidi, Serikali imepunguza gharama kwa wachimbaji kwa kupunguza kiwango cha mrabaha kutoka asilimia 6 hadi 4, na kuondoa ada ya huduma kutoka asilimia 1 hadi 0, hatua iliyolenga kuwahamasisha wachimbaji kuuza hata hadi asilimia 100 ya dhahabu yao kwa Benki Kuu.
Katika kutekeleza mpango huu, BoT inashirikiana na viwanda vitatu vya uchenjuaji dhahabu vilivyopo nchini ambavyo ni Geita Gold Refinery (GGR) ya Geita, Mwanza Precious Metals Refinery ya Mwanza, na Isographica Refinery ya Dodoma. Wachimbaji wanahimizwa kupeleka dhahabu yao kwenye viwanda hivi kwa ajili ya usafishaji kabla ya kuuzwa rasmi kwa BoT, kulingana na ukaribu wa eneo wanakofanyia shughuli zao.
Kupitia mpango huu, BoT inakusudia kuimarisha hifadhi ya dhahabu ya taifa (gold reserves), hatua inayochangia katika uthabiti wa thamani ya shilingi, uhimilivu wa uchumi wa taifa dhidi ya misukosuko ya kiuchumi ya kimataifa, na pia kuongeza uwezo wa Serikali katika mipango ya maendeleo kwa kutumia fedha za kigeni zitokanazo na dhahabu.
Ushiriki wa Benki Kuu katika maonesho haya ni sehemu ya mkakati mpana wa utoaji wa elimu kwa umma kuhusu majukumu yake katika sekta ya fedha na uchumi, huku ikionyesha namna taasisi hiyo inavyoshirikiana na wadau mbalimbali kukuza uchumi wa taifa kupitia sekta ya madini.


