Msukuma Apongeza Maonesho ya Teknolojia ya Madini Geita



Na Humphrey Msechu, Geita

Aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Geita Vijijini ambaye pia anawania tena nafasi hiyo, Joseph Kasheku Msukuma, ameipongeza Kamati ya Maandalizi ya Maonesho ya Nane ya Teknolojia ya Madini yanayofanyika katika viwanja vya Samia Suluhu Hassan, mkoani Geita.

Msukuma alisema wazo la kuanzisha maonesho hayo lilianza kipindi chake akiwa Mbunge, akishirikiana na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa huo, Mhandisi Robert Gabriel, ambapo mara ya kwanza yalifanyika kwenye uwanja wa mpira na mwaka uliofuata walijenga jengo la utawala.

“Leo hii tunashuhudia maonesho haya yakiendelea kusonga mbele huku idadi ya washiriki ikiongezeka kila mwaka. Hili linatupa moyo kuona wananchi na wadau wanaitikia kwa wingi,” alisema Msukuma.

Mbali na kuipongeza Kamati ya Maandalizi, Msukuma pia aliisifu kampuni ya FEMA Mining, akisema ni mfano bora wa mchango wa sekta binafsi katika kuendeleza sekta ya madini na jamii kwa ujumla. Alibainisha kuwa kupitia ushirikiano na serikali za mitaa, kampuni hiyo imekuwa ikitoa fedha za Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) kati ya shilingi milioni 159 hadi 400.

Kwa upande wake, Afisa Usalama wa FEMA Mining, Victor Mkono, alisema kampuni hiyo ya uchimbaji inayoendesha shughuli katika mgodi wa Buckreef ni ya Kitanzania na inamilikiwa na Watanzania kwa asilimia 100.

“Tumejipanga kuhakikisha sehemu ya mapato tunayopata inarudi kwenye jamii, hususan kwenye sekta ya afya, elimu, pamoja na kuchimba visima virefu vya maji safi na salama kwa wananchi,” alisema Mkono.

Maonesho ya Teknolojia ya Madini Geita yameendelea kuwa jukwaa muhimu la kuonyesha mchango wa sekta hiyo katika kukuza uchumi na kuboresha maisha ya wananchi.
Previous Post Next Post