GCLA KUENDELEA KUSIMAMIA MATUMIZI SALAMA YA KEMIKALI KATIKA SEKTA YA MADINI



Na mwandishi wetu, Geita

Meneja wa Kanda ya Ziwa wa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, John Faustine, ameupongeza uanzishwaji wa maonyesho ya madini yanayofanyika katika mkoa huu, akisema ni fursa muhimu kwa wadau wa sekta ya madini kujifunza na kupata mwongozo wa kitaalamu juu ya matumizi salama ya kemikali.

Akizungumza kwenye maonyesho hayo, Faustine alisema kuwa mamlaka hiyo ipo kwa lengo la kuhakikisha wadau wanaojishughulisha na madini na kemikali wanafuata sheria na kanuni zinazohusiana na usalama wa binadamu na mazingira. “Mkemia Mkuu wa Serikali ana jukumu la usajili wa kemikali zote nchini, kutoa vibali vya kuingiza na kusafirisha kemikali, pamoja na kusajili wadau na maeneo wanayoyatumia kemikali,” Faustine alisema.

Faustine alisema kuwa mamlaka inatekeleza majukumu mawili makuu: usimamizi wa sheria za kemikali na uchunguzi wa kimaabara wa ubora na usalama wa kemikali. “Sheria ya Udhibiti na Usimamizi wa Kemikali Majumbani, ya mwaka 2003, ni muhimu sana kwa sababu shughuli nyingi za binadamu zinahusisha kemikali. Kwa hivyo, ni lazima kuwe na miongozo inayotekeleza matakwa ya sheria hizi,” alisema.

Aliongeza kuwa katika uchenjuaji wa madini kama dhahabu, ni muhimu kwa wachimbaji kuelewa kiwango cha dhahabu kilichopo kwenye udongo na madini yanayoweza kushindana na kemikali zinazotumika. “Kemikali hizi zina tabia ya ‘kutafuna’ madini pale zinapokuwa zikitumika. Hivyo, wachimbaji wanashauriwa kupeleka udongo wao kwenye maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kabla ya kuanza uchenjuaji ili kubaini kiasi cha dhahabu na madini jirani kama silva, kopa, na salfa, ili uchenjuaji uwe rahisi na salama,” Faustine alisema.

Mamlaka hiyo pia imewatoa wito wadau wote wa kemikali kuhakikisha wanatumia kemikali kwa taratibu salama. Faustine alisisitiza kuwa matumizi mabaya ya kemikali yanaweza kuathiri afya ya binadamu, jamii na mazingira. “Kemikali ikishaingia ardhini haina mpaka. Hivyo ni jukumu letu sote kuhakikisha mazingira yetu na jamii ziko salama,” alisema.

Maonyesho hayo yamekuwa pia ni jukwaa la wadau kujifunza na kutatuliwa changamoto zao na wataalamu wa mamlaka, huku ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali ikitoa mwongozo wa kitaalamu kwa wachenjuaji na wadau wengine wanaojishughulisha na madini.
Previous Post Next Post