Benki ya CRDB imeendelea kuwazawadia wateja wake wanaotumia huduma za kidijitali kupitia kampeni ya SimBanking, ambapo mshindi wa pili wa gari jipya aina ya IST, Fahad Soud kutoka Tanga, amekabidhiwa zawadi yake jijini Dares Salaam.
Hafla ya makabidhiano hayo imefanyika katika viwanja vya Dar Village, Mikocheni, ikihudhuriwa na viongozi waandamizi wa benki hiyo, wadau wa sekta ya fedha pamoja na wateja wa CRDB.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mkuu wa Kitengo cha Wateja Binafsi wa CRDB, Stephen Adili alisema kampeni ya SimBanking inalenga kuhamasisha matumizi ya huduma za kifedha kidijitali miongoni mwa Watanzania.
"Kampeni hii ni sehemu ya mkakati wetu wa kuongeza ujumuishi wa kifedha na kuwahamasisha wateja kutumia huduma za kidijitali kama SimBanking. Zawadi ni motisha kwa wateja wetu, lakini pia ni njia ya kurudisha fadhila kwa kuwaunga mkono," alisema Adili.
Aliongeza kuwa mbali na magari ya kila mwezi, zawadi nyingine zinazotolewa ni pamoja na fedha taslimu, ufadhili wa masomo kwa wanafunzi wa vyuo, na zawadi nyingine nyingi, ambapo mteja huhitaji tu kuwa amejiunga na SimBanking na kufanya miamala mbalimbali kama kununua umeme, kulipia bili, au kukata tiketi za treni ya SGR.
Kwa upande wake, mshindi wa zawadi ya gari aina ya IST, Fahad Soud, aliishukuru CRDB kwa kampeni hiyo na kusema ushindi huo umebadilisha maisha yake kwa kiwango kikubwa.
“Sikutarajia kabisa kushinda. Hii ni ndoto kuwa kweli! Nawaomba Watanzania wengine wasisite kutumia SimBanking kwani ushindi ni wa kweli kabisa,” alisema Soud kwa furaha.
Benki ya CRDB imebainisha kuwa kampeni hiyo itaendelea hadi Desemba mwaka huu, ambapo mshindi wa mwisho atazawadiwa gari kubwa aina ya Harrier Anaconda huku zawadi nyingine zikiendelea kutolewa kila mwezi.