TAMWA YAWAJENGEA UWEZO WANAHABARI KUHUSU USALAMA MTANDAONI KUELEKEA UCHAGUZI MKUU 2025






 Na Lilian Ekonga Dar es Salaam,  


Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) kimeendelea na juhudi zake za kuwawezesha waandishi wa habari kwa kuwapatia mafunzo maalum kuhusu usalama mtandaoni, ikiwa ni sehemu ya maandalizi kuelekea Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu.

Mafunzo hayo yamelenga kuwapa wanahabari maarifa ya kujilinda dhidi ya vitisho vya kidijitali na kuboresha utayarishaji wa maudhui yenye maadili, yanayozingatia ukweli na kuepusha uchochezi katika kipindi nyeti cha uchaguzi.

Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo yaliyofanyika leo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA, Dkt. Rose Reuben, alisisitiza kuwa usalama wa wanahabari ni nguzo muhimu katika kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa uwazi, amani na uadilifu.

"Usalama wa waandishi wa habari, hususan usalama wa mtandaoni, ni muhimu sana wakati huu wa kuelekea uchaguzi. Wanahabari wanapokuwa salama, wanaweza kutekeleza majukumu yao kwa weledi, uhuru na ufanisi mkubwa," amesema Dkt. Rose.


Dkt. Rose alieleza kuwa mafunzo hayo ni sehemu ya mikakati ya TAMWA ya kuhakikisha wanahabari, hasa wanawake, wanapata uelewa wa kutosha juu ya namna ya kujilinda dhidi ya hatari za kidijitali kama vile udanganyifu, mashambulizi ya kimtandao, na unyanyasaji.

Aidha, alihimiza matumizi ya mitandao ya kijamii kwa uwajibikaji, akibainisha kuwa wanahabari wana wajibu mkubwa wa kuhakikisha wanatoa habari sahihi na zisizoleta taharuki kwa jamii.

"Katika kipindi hiki, hatuwezi kubeza athari za habari potofu. Ni jukumu la kila mwanahabari kuhakikisha anazingatia ukweli, uadilifu na weledi katika kazi yake ya kuripoti masuala ya uchaguzi," aliongeza.




Mafunzo hayo yamegusa maeneo muhimu ya usalama mtandaoni ikiwemo: mbinu za kujikinga dhidi ya mashambulizi ya kimtandao, matumizi salama ya mitandao ya kijamii, na mikakati ya kukabiliana na vitisho vya kidijitali vinavyolenga waandishi wa habari.

Baadhi ya waandishi wa habari waliopata mafunzo hayo walieleza kufurahishwa na maarifa waliyoyapata, wakisema yatawasaidia kuongeza ufanisi na usalama katika utendaji wao hasa wakati huu wa kuelekea uchaguzi.

Mafunzo haya yamekuja katika kipindi nyeti cha maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa 2025, ambapo waandishi wa habari wanatarajiwa kuwa mstari wa mbele katika kufikisha taarifa sahihi kwa wananchi na kusaidia kulinda amani ya taifa.










Previous Post Next Post