Na Mwandishi wetu....
Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Jaji wa Mahakama ya Rufani Jacobs Mwambegele, ametoa wito kwa wazalishaji wa maudhui mtandaoni kuhakikisha kuwa taarifa wanazochapisha katika kurasa zao ni za kweli, sahihi, na hazina chembe ya upotoshaji ili kulinda amani na utulivu wa nchi.
Jaji Mwambegele alitoa kauli hiyo leo, Agosti 3, 2025, jijini Dar es Salaam wakati akifungua mkutano wa kitaifa baina ya INEC na wazalishaji wa maudhui mtandaoni, unaolenga maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
"Nawasisitiza na kuwakumbusha juu ya umuhimu wa kuepuka matumizi mabaya ya akili bandia, ambayo inatumiwa na baadhi ya watu wenye nia ovu kusambaza habari za upotoshaji, hususan kupitia mitandao ya kijamii," alisema Jaji Mwambegele.
Aidha, Mwenyekiti huyo alieleza kuwa INEC ina matumaini makubwa na vyombo vya habari katika kufanikisha uchaguzi wa mwaka huu, kutokana na mchango mkubwa walioutoa katika hatua mbalimbali, zikiwemo za uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
"Imani hii inatokana na ushirikiano wenu mliouonesha tangu awali kwenye zoezi la uboreshaji wa daftari la wapiga kura. Mmeendelea kuwasilisha hoja na ushauri kila tunapokutana kwenye vikao," aliongeza.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Uchaguzi Ramadhan Kailima aliwasilisha mada kuhusu maandalizi ya uchaguzi na kuhimiza vyombo vya habari kutumia kalamu na majukwaa yao kusambaza ujumbe wa amani na kutoa taarifa sahihi kwa umma.
"Tunawaomba na kuwasihi, kutumia nafasi na fursa mlizonazo kuhakikisha kunakuwepo na taarifa za mara kwa mara za kuelezea kinachoendelea kuhusu uchaguzi," alisema Kailima.
Aliongeza kuwa vyombo vya habari vina nafasi ya kipekee kuwa mstari wa mbele katika kubaini na kufichua upotoshaji unaoweza kufanyika kwa bahati mbaya au kwa makusudi dhidi ya Tume au mchakato mzima wa uchaguzi.
"Tume imejiwekea utaratibu wa kuvishirikisha vyombo vya habari katika mchakato mzima wa uendeshaji wa uchaguzi huu, ili kuweka uwazi na kuhakikisha wanashiriki kikamilifu," alisema kwa kusisitiza.
Mkutano huo umetajwa kuwa sehemu ya juhudi za kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa uwazi, amani, na ushirikiano kati ya wadau wote muhimu.