Na mwandiahi wetu...
Mkurugenzi wa VETA, CPA Anthony Kasore, asema watoto wadogo wanapaswa kuanza kujifunza ujuzi mapema ili kuwa na ufanisi katika maisha ya baadaye.
Leo, tarehe 7 Julai 2025, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi stadi (VETA)Anthony, amesisitiza umuhimu wa kuanzisha watoto wadogo kwenye ujuzi wa maisha mapema ili kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi na kijamii. Akizungumza na waandishi wa habari, Mkurugenzi huyo alieleza kuwa mfumo wa elimu nchini umeendelea kuboreshwa ili kutoa fursa kwa kila mtoto kupata elimu ya vitendo inayoweza kumuwezesha kujitegemea na kuleta mabadiliko kwa jamii.
Akizungumzia sera mpya ya elimu, Kasore alisema kuwa katika mwaka 2023, Serikali ilifanya maboresho kwenye sera ya elimu, na mwaka huu, Rais wa Tanzania alizindua rasmi sera hiyo ya elimu ya ufundi stadi. Sera hii inasisitiza kuanzisha ujuzi kwa watoto kuanzia ngazi ya shule za msingi na sekondari, ambapo wanafunzi watajifunza mbinu za ubunifu na ujasiriamali.
Mkurugenzi huyo aliongeza kuwa lengo la VETA ni kutoa elimu itakayowasaidia Watanzania kupata ujuzi utakao wawezesha kujiajiri na kushiriki katika uchumi wa nchi. Alisisitiza kuwa ni muhimu kutoa elimu ya ujuzi inayohusisha ubunifu ili watoto wa kizazi cha sasa waweze kuzalisha bidhaa na kufanya biashara zao wenyewe, huku wakijua umuhimu wa kuingia kwenye soko la ajira na kujenga ustawi wao.
"Watoto wanapokuwa na ujuzi wa vitendo, wanakuwa na uwezo wa kujiajiri au kujitengenezea fursa za ajira. VETA inatoa mafunzo yanayowasaidia wanafunzi kuunda na kuuza bidhaa, na hiyo inajumuisha pia mbinu za ujasiriamali ili waweze kufanya biashara zao kwa ufanisi," alisema Kasore.
Katika jitihada za kutekeleza sera hii, VETA imeanzisha maeneo maalum ya kutoa elimu ya ujuzi kwa watoto na vijana. Hizi ni fursa muhimu kwa watoto kujifunza mbinu za ujasiriamali, kutengeneza bidhaa, na kuanza biashara zao wenyewe. VETA pia imejizatiti katika kuleta mabadiliko kwa kuonesha umuhimu wa ujuzi katika maendeleo ya taifa, kama sehemu ya sera ya elimu ya Tanzania ambayo inalenga kutoa elimu kwa wote, kuanzia ngazi ya shule ya msingi hadi sekondari.
VETA imejizatiti kutoa elimu ya ufundi na ujasiriamali kwa watoto na vijana ili kuwawezesha kujitengenezea fursa za ajira katika jamii. Kwa sasa, elimu hiyo inatolewa kwa umakini mkubwa, na kila mtoto anajengewa uwezo wa kubuni, kutengeneza na kuuza bidhaa mbalimbali.
Kwa kumalizia, Mkurugenzi wa VETA alisisitiza kuwa, "Tunajivunia kuona mabadiliko makubwa katika mfumo wa elimu ya Tanzania. VETA, kwa kushirikiana na Serikali, tutaendelea kuwekeza katika mafunzo ya ujuzi ili kuhakikisha vijana wetu wanakuwa na uwezo wa kujiajiri na kuleta mabadiliko chanya katika jamii na uchumi wa taifa letu."