Na Mwandishi wetu.....
Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) imesema kuwa shughuli za utafutaji, uendelezaji na uzalishaji wa mafuta na gesi asilia nchini zimeendelea kuimarika chini ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
PURA imebainisha hayo Mei 19, 2025 kupitia Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Mhandisi Charles Sangweni wakati wa kikao na wahariri na waandishi wa habari kilichofanyika Jijini Dar es Salaam kilicholenga kuelelezea utekelezaji wa majukumu ya PURA na mafanikio yaliyopatikana chini ya Serikali ya Awamu ya Sita.
Miongoni mwa mafanikio aliyotaja Sangweni ni pamoja na kutoa ushauri kwa Serikali kuhusu masuala yanayohusiana na shughuli za mkondo wa juu wa petroli uliowezesha,kutolewa kwa leseni ya uendelezaji katika eneo la ugunduzi la Ntorya,
kufanyika kwa ukarabati wa visima vitano vya uzalishaji gesi asilia ambao umepelekea kuimarika kwa uzalishaji wa gesi asilia, kuchukuliwa kwa data za mitetemo katika vitalu vya Ruvu na Ruvuma; na
kufanyika kwa tafiti za awali za kijiolojia, kijiofizikia na kijiokemia katika utafutaji wa mafuta na gesi asilia.
Mafanikio mengine ni PURA kuimarisha uthibiti wa shughuli za uhakiki na kaguzi za mikataba ya uzalishaji na ugawanaji wa mapato; kuongezeka kwa ushiriki wa wazawa katika shughuli za mkondo wa juu wa petroli; na kuimarisha mfumo wa udhibiti kwa kuandaa na kuboresha kanuni na miongozo mbalimbali ya kisheria.
Kwa upande wa uzalishaji wa gesi asilia, Sangweni amesema kuwa kwa kipindi cha miaka minne kuanzia Machi 2021 hadi Machi 2025, kiasi cha gesi asilia kilichozalishwa kimefikia futi za ujazo Bilioni 301.33.
Katika eneo la ukaguzi wa gharama za mikataba ya uzalishaji na ugawanaji mapato, Sangweni amesema kuwa katika kipindi husika PURA imewezesha kurejeshwa kwa zaidi ya Shilingi bilioni 340 kwenye mfuko wa ugawanaji wa mapato kati ya Serikali.
Vile vile, kupitia udhibiti unaofanywa na PURA, ushiriki wa watanzania katika miradi ya mkondo wa juu petroli umeongezeka maradufu.