Na Lilian Ekonga......
Katika kuimarisha Huduma za Afya ya Uzazi nchini
Klabu ya Riadha ya 'The Runners, imetoa vifaa tiba kwa wanawake wajawazito na watoto wachanga katika Hospitali ya Mnazi jijini Dar es salaam.
Vifaa hivyo ni kipimajoto cha kidigitali, seti za sindano maalum (cannulas), na kifaa cha kufuatilia afya ya mtoto tumboni (fetal monitor)
Akizungumza na Waandishi wa habari wakati wa hafla ya makabidhiano, msemaji wa klabu hiyo, Godphrey Mindu, amesema kuwa vifaa hivyo ni kwa ajili ya watoto walioko tumboni,waliotoka kuzaliwa pamoja na wanawake wajawazito.
Ameongeza kuwa vifaa hivyo vimetolewa kama sehemu ya kuiunga mkono serikali na Rais Samia Suluhu Hassan katika juhudi zake za kuboresha huduma ya mama na mtoto na kuhakikisha usalama wa mama wajawazito na watoto wao
“Tumetoa vifaa hivi kwa sababu tunatambua changamoto zinazowakabili wahudumu wa afya, hasa katika wodi ya uzazi ni upatikanaji wa vifaa vya kutosha kwa sababu watoto wanazaliwa kila muda," amesema Mindu.
Alitoa wito kwa wadau wengine kuungana na serikali kuboresha huduma ya afya kwa ajili ya kuokoa maisha ya wengine.
Kwa upande wake, Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo, Dk Linda Mutasa, alieleza kuwa msaada huo umekuja wakati muafaka kwa sababu kulikuwa na upungufu wa vifaa hivyo vya huduma ya dharura kwa wanawake wajawazito na watoto.
“Vifaa hivi vitatusaidia kuboresha ufuatiliaji wa afya ya mama na mtoto kuanzia akiwa tumboni, wakati wa kuzaliwa na baada ya kuzaliwa na kusaidia kuokoa maisha yao kwa hiyo tunashukuru sana kwa msaada huu,” alisema Dk Mutasa.
Naye Meneja wa Masuala Endelevu wa Matukio kutoka Benki ya Absa, Abigael Lukuvi amesema benki hiyo itaendelea kushirikiana na klabu hiyo kusaidia sekta ya afya kupitia matukio mbalimbali yajayo.
“Kwa kila tukio tutakaloshiriki na Klabu ya Riadha, tutaweka mkazo kuhakikisha Mnazi Mmoja inapokea vifaa bora zaidi kwa sababu upendo kwa jamii ndiyo msingi wa ustawi wa taifa,” amesema Lukuvi.
Amesema klabu ya hiyo imekuwa mstari wa mbele katika kushirikiana na serikali uboresha huduma za afya kupitia matukio ya kijamii na michezo, ikiwa ni sehemu ya jitihada zake za kuchangia maendeleo ya jamii.