VIJANA WAHAMASISHWA KUJITOKEZA UBORESHAJI WA DAFTARI LA MPIGA KURA AWAMU YA PILI.



Katibu wa Idara ya Chipukizi na Uhamasishaji wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Taifa, Jesca Mshana, ametoa wito kwa vijana wa Kitanzania kujitokeza kwa wingi kushiriki katika zoezi la kuboresha Daftari la Kudumu la Mpiga Kura awamu ya pili, linalotarajiwa kuanza Mei 1 hadi 7, 2025.

Akizungumza na vyombo vya habari, Mshana alisema kuwa ni muhimu kwa vijana kutambua nafasi yao katika mustakabali wa taifa, kwa kuhakikisha wanajiandikisha ili wapate haki ya msingi ya kupiga kura. “Kupiga kura ni haki ya msingi na sauti ya mabadiliko. Vijana msikose kushiriki kwenye hatua hii muhimu ya kidemokrasia,” alisisitiza.

Alieleza kuwa mchakato huo utaanza katika mikoa ya Geita, Mwanza, Ruvuma, Mbeya na Songwe, kabla ya kuhamia kwenye mikoa mingine 16 ikiwemo Dar es Salaam, Arusha na Kilimanjaro. Vilevile, kuanzia Mei 16 hadi 22, uboreshaji utaendelea katika vyuo vya elimu ya juu pamoja na vituo vya magereza.

Aidha, Mshana aliwataka vijana wajitokeze kugombea nafasi mbalimbali za uongozi, akisisitiza kuwa taifa linahitaji fikra mpya na uongozi wenye dira kutoka kwa vijana. “Tunahitaji mawazo mapya. Vijana waonesheni uwezo wenu kwa kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali ili kubeba ajenda za maendeleo kwa vizazi vya sasa na vijavyo,” alieleza.

Kwa msisitizo zaidi, aliwakumbusha vijana kuwa uvivu wa kushiriki mchakato wa uchaguzi huacha nafasi kwa watu wasiokuwa na dhamira njema kuongoza taifa. “Kukaa kimya ni kuruhusu mustakabali wenu kuamuliwa na wengine,” aliongeza.




Katika hitimisho la hotuba yake, Jesca Mshana alisisitiza umuhimu wa kudumisha amani ya taifa, akisema kuwa UVCCM na Chipukizi hawatakubali kuona amani ya nchi inavurugwa. “Tunaamini katika misingi imara ya waasisi wa taifa hili, na viongozi wa sasa wanaendeleza hilo. Amani ni urithi wetu, na vijana tuna jukumu la kuilinda kwa gharama yoyote,” alisema kwa msisitizo.

Zoezi hilo la uboreshaji wa daftari ni sehemu ya maandalizi kuelekea uchaguzi mkuu, ambapo ushiriki wa vijana unaendelea kusisitizwa kama nguzo muhimu ya ujenzi wa taifa.





Previous Post Next Post