Na Mwandishi Wetu, Arusha
TAASISI ya Elimu Tanzania (TET) imetoa rai kwa wazazi na walezi wenye watoto wanaosoma madarasa ya awali, msingi, sekondari ,vyuo pamoja na watu wenye mahitaji maalum kununua vitabu vya mitaala mipya vinavyopatikana katika taasisi hiyo na kuuzwa maeneo mbalimbali nchini.
Rai hiyo imetolewa leo Machi 3,2025 jijini Arusha na Mkuza Mtaala wa TET, Zena Amiri alipozungumza na wananchi wanaoendelea kufika katika banda la taasisi hiyo kununua vitabu vya mitaala iliyoboreshwa.
Vitabu hivyo vinapatikana kwa bei nafuu ndani ya banda hilo kupitia kampeni iitwayo 'Kitabu Kimoja, Mwanafunzi Mmoja'.
Amesema taasisi hiyo inajukumu kubwa la kutafsiri sera ya elimu na kutengeneza mtaala bora huku akiendelea kufafanua kazi nyingine za TET kwamba ni kufanya tafiti mbalimbali, kuandaa mtaala wa elimu na vifaa pia kutoa mafunzo elekezi kwa viongozi wa elimu katika makundi mbalimbali ikiwemo wanafunzi, walimu, wazazi na makundi maalum.
"Mitaala iliyoboreshwa inalengo la kutoa elimu nyumbufu ambayo inamfanya mwanafunzi kusoma na kuenda katika taaluma yake husika na katika maonesho haya ya Siku ya Wanawake Dunia yenye kauli mbiu Wanawake na Wasichana 2025 tuimarishe Haki, Usawa na Uwezeshaji"
Naye Hadija Salumu mhakiki wa vitabu vya maandishi ya breli amesema katika taasisi hiyo wanapigachapa vitabu vya maandishi ya breli kwa shule za msingi, sekondari na vyuo ili kuwasaidia wanafunzi wasioona kusoma maandishi hayo hivyo alisisitiza wazazi na walezi kuwapeleka watoto wao shule ili waweze kusoma na kutimiza ndoto zao
Wakati huohuo Mkuza Mitaala wa somo la kifaransa kutoka TET, Maria Jeremia alisisitiza katika maadhimisho ya wiki ya wanawake taasisi hiyo inahamasisha wananchi kununua vitabu ikiwemo vitabu kwa watoto wasioona ili nao waweze kufikia malengo yao.
Mwishoooo