Na Lilian Ekonga........
Taasisi ya Alhikma Foundation, kupitia Mashindano yake ya Qur’aan Tukufu yaliyofanyika Machi 16, 2025, imetangaza kufanikisha ndoa za vijana 200 wasio na uwezo wa kulipa mahari—100 kutoka Tanzania na 100 kutoka Burundi. Lengo la mpango huu ni kusaidia vijana wenye nia ya kuoa lakini wanakabiliwa na changamoto za kifedha.
Aidha, taasisi hiyo imetangaza mpango wa kuwafanyia tohara watoto wa kiume 1,000, huku wengine 50 wakidhaminiwa na Hospitali ya Polyclinic, hivyo kufanya jumla ya watoto 1,050 watakaonufaika na huduma hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa Alhikma Foundation, Sheikh Nurdeen Kishki, ameishukuru jamii ya Watanzania kwa kufanikisha mashindano hayo kwa amani na kwa kushiriki kwa wingi.
Sheikh Kishki ameeleza kuwa kuanzia Aprili 10 hadi Aprili 30, 2025, kwa muda wa siku 20, fomu za maombi ya ndoa zitapatikana katika makao makuu ya Alhikma Foundation. Waombaji watatakiwa kuchukua, kujaza, na kurejesha fomu hizo, baada ya hapo jopo maalum litafanya mchujo na usaili wa mwisho kabla ya kutangaza rasmi ndoa hizo.
Kwa upande wa watoto wa kiume 1,050 watakaofanyiwa tohara, Sheikh Kishki amesema zoezi hilo litasimamiwa na jopo la madaktari wenye uzoefu, wakitumia mbinu za kisasa kuhakikisha usalama na ustawi wa watoto hao.
Sheikh Kishki Pia amesema City College imetoa nafasi za masomo kwa vijana 50 wa Kitanzania kupitia udhamini wa Alhikma Foundation. Kwa yeyote anayependa kusomea taaluma ya afya kupitia City College, hususan katika kampasi yake ya Ilala, fursa hiyo itaanza kupatikana tarehe 10 Aprili kwa kufuata taratibu za maombi katika ofisi za Alhikma Foundation.
Sheikh Kishki pia amewashukuru Watanzania na viongozi wote walioshiriki katika Mashindano ya Qur’an kwa kujaza Uwanja wa Taifa na kuifanya Tanzania kujulikana kwa mwitikio mkubwa wa kushiriki mashindano hayo.