Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Prof. Palamagamba Kabudi akitoa hotuba wakati akifungua Mkutano wa Mwaka wa Vyombo vya Utangazaji unaofanyika katika ukumbi wa New Generation Dodoma Februari 13 na 14,2025.
Picha na Kadama Malunde
Waziri Kabudi Awasihi Vyombo vya Utangazaji Kutumia Kiswahili Fasaha ili Kukinga Uharibifu wa Lugha
NA NEEMA NKUMBI -DODOMA
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Prof. Palamagamba Kabudi, amekemea matumizi ya Kiswahili kisichofasaha katika vyombo vya utangazaji, akisisitiza kuwa vyombo vya habari viache "kubananga" lugha ya Kiswahili.
Akizungumza katika ufunguzi wa Mkutano wa Mwaka wa Vyombo vya Utangazaji, Waziri Kabudi amesema kuwa matumizi mabaya ya Kiswahili yanaathiri uwezo wa Watanzania kuzungumza lugha hiyo kwa ufasaha.
Prof. Kabudi amekosoa matumizi ya maneno kama "apa" badala ya "hapa" na "uyu" badala ya "huyu," ameonya kuwa uharibifu huu wa lugha unawaathiri wananchi na kusababisha Kiswahili kisicho fasaha kutumika zaidi.
Amesisitiza kuwa sekta ya utangazaji ina jukumu kubwa la kuhabarisha umma na kwamba ni muhimu kuzingatia matumizi sahihi ya Kiswahili sanifu ili kulinda hadhi ya lugha hiyo.
Waziri ameeleza kuwa, vyombo vya habari vinapaswa kuepuka matumizi ya maneno ya Kiswahili ambayo yana maana isiyo sahihi na kuongeza kuwa, Kiswahili cha kisasa kimeathiriwa na makosa ya watangazaji.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa vyombo vya habari kutoa vipindi vya manufaa kwa jamii, ikiwemo kuelimisha kuhusu mabadiliko ya tabia nchi, na kuwaonya waandishi wa habari kutumia taaluma zao kwa usahihi, hasa katika kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA)Dkt. Jabir Bakari, amesema wameandaa mkutano huo ili kujadili masuala ya sekta ya habari pamoja na kutafuta ufumbuzi wa changamoto ambazo bado zinaikabili sekta hiyo.
Akizungumzia Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika mwaka huu, amewasihi waandishi wa habari kutumia taaluma yao vizuri kwa kuhabarisha umma juu ya hatua zote za uchaguzi Mkuu hadi siku ya kupiga kura.
Baadhi ya washiriki wa mkutano huo Samuel Samsoni amesema "Vyombo vya habari vina nafasi kubwa ya kuelimisha jamii na kufikisha taarifa kwa jamii, ni wajibu wa mamlaka husika kushirikiana na vyombo vya habari kufikisha elimu hiyo kwa jamii huku wakivisaidia vyombo vya habari kufikia malengo yanayotarajiwa na mamlaka na kuepuka taarifa za upendeleo na uchawa".