Na Mwandishi wetu.....
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira, na wenye ulemavu) Ridhiwan Kikwete amewata Vijana kushiriki kikamilifu katika uhakiki wa Rasimu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kwa kutoa maoni muhimu yanayowagusa.
Wito huo ameutoa leo Disemba 18, 2024 jijini Dar es Salaam katika Mkutano na Mtandao wa Vijana Kuhakiki Rasimu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ulioandaliwa na Tume ya Mipango.
Amesema vijana wanapaswa kusema Tanzania wanayoitaka na serikali ipo tayari kusikiliza maoni yao na kuyafanyia kazi.
“Endeleeni kushiriki katika mijadala hii ya kutoa maoni yenu kuhusu Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ikiwemo kubainisha mambo ambayo dira hiyo haijayazungumzia pamoja na kushauri maboresho yanayopaswa Kufanyika ili kuhakikisha kuwa masuala yenu yanawasilishwa ipasavyo.
“Elezeni pia yale ambayo mnaona hayakuelezwa vizuri na kueleza Tanzania mnayoitaka. Na mnapotoa maoni yenu msijiangalie nyinyi tu, angalieni pia na vizazi vijavyo,” amesema Kikwete.
Ameongeza kuwa serikali imeendelea kuwekeza katika maeneo mengi kama vile elimu, afya, na mambo yote ya ustawi wa jamii ili kuhakikisha vijana wanafaidika.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa mipango kitaifa kutoka Tume ya Mipango, Anjela Shayo amesema uwepo wa vijana katika uhakiki wa Rasimu hiyo ni kuhakikisha yale mambo makuu yanayohusu vijana kama yamezingatiwa.
Amesema timu ya uandishi wa dira ya 2050 imejipanga kupokea maoni kutoka kwenye makundi mbalimbali lengo kuhakikisha wanafikia kila kundi.
“Sisi tunaamini Dira hii ni ya vijana kwani asilimia 80 ya maoni tuliyoyapokea yametoka kwa vijana kwani wao ndio wenye mambo mengi ikiwemo uchumi jumishi, Ajira,uwezeshaji na mazingira wezeshi ya biashara haya yote yanamgusa kijana na ndio maana tunasema dira hii ni ya vijana”,amesema.
Aidha ameongeza kuwa vijana waliokutana nao ni kutoka sehemu mbalimbali nchini hivyo lengo la kupata maoni kutoka kwa vijna litatimia na wanatarajia kupata maoni mengi yenye kujenga.
Akitoa maoni yake, Mkurugenzi Mtendaji wa Binti Salha Foundation, Salha Aziz amesema kuelekea 2050 ni muhimu Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ikaainiaha wazi mikakati mahususi ya kuweza kupambana na tatizo la ajira kwa vijana kwa kuwa na program za kushughulikia changamoto mbalimbali zinazokwamisha vijana kujiajiri pamoja na ajira kwa vijana.
“Ni muhimu serikali kushughulikia changamoto na malalamiko ya vijana wanaofanya biashara ndogondogo nchini pamoja na wale wanaoanzisha biashara mpya, kwani biashara nyingi zinakutana na vikwazo vinavyokwamisha biashara hizo kuweza kukua,” amesema Salha.
Naye Mkurugenzi wa Shirika la The African Leadership Initiative for Impact, Joseph Malekela amesema ni vyema Dira hiyo ikaainisha namna ambavyo inawaandaa vijana kuweza kushuka nafasi mbalimbali za kimaamuzi, pamoja na kuwaandaa kuweza kuzitumia nafasi hizo kwa uadilifu na uzalendo.