Na Mwandishi wetu.......
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kivukoni Kinondoni imemuachia huru Mkurugenzi wa Msama Promotion, Alex Msama baada ya upande wa Jamhuri kushindwa kuthibitisha mashtaka ya kughushi nyaraka za kiwanja dhidi yake.
Katika kesi hiyo ya jinai namba 275 ya mwaka 2022 imetolewa hukumu leo na Hakimu Mkazi Mfawidhi, Isihaka Kupwa ambapo Msama alikuwa anakabaliwa na mashtaka matano.
Hakimu Kupwa alisema mahakama hiyo ilipokea na kupitia vielelezo na ushahidi wa pande zote mbili pasina kuacha.
Hakimu Kupwa amesema baada ya mahakama hiyo kupitia ushahidi wa pande zote mbili, imeona upande wa Jamhuri umeshindwa kuthibitisha mashtaka dhidi yake hivyo inamuachia huru na kumpa ushindi.
Miongoni kwa sababu alizozitaja Hakimu Kupwa ni kwamba Jamhuri ilishindwa hata kuwasilisha cheti cha kifo cha marehemu aliyetajwa katika kesi hiyo, pia kukosekana kwa mtaalamu wa kuthibitisha maandishi yaliyoghushiwa.
“Mahakama hii inamuachia huru Alex Msama Mwita, haki ya kukata rufaa ipo wazi,”.
Miongoni mwa mashtaka yaliyokuwa yakimkabili Msama ni Kughushi, ambapo anadaiwa siku isiyojulika ndani ya Jiji la Dar es Salaam kwa nia ya kufanya udanganyifu alighushi nyaraka za mauziano yenye Tarehe ya Julai 6, 1970, akikusudia kuonyesha kuwa ni nyaraka halisi za mauziano kati ya Khalid Swalee Chengu na Ndelikyama Mweleli huku akijua fika kuwa ni za uongo.
Pia shtaka jinginr inadaiwa Aprili 24, 2016 ndani ya Jiji la Dar es Salaam Kwa nia ya kufanya udanganyifu, anadaiwa kughushi sahihi ya Ndelikyama Mabolio Mweleli katika Mkataba wa mauzo wa Aprili 24, 2016 Kwa kusudi la kuonyesha kuwa ni nyaraka halisi za mauziano kati yake na Ndelikyama Mabolio Mweleli, huku akijua wazi kuwa ni uongo.
Pia inadaiwa siku ya Aprili 24, 2016 ndani ya Jiji la Dar es Salaam, Kwa nia ya kufanya udanganyifu, alighushi barua ya ofa yenye kumbukumbu namba D/KN/A/13504/TMM yenye Tarehe ya Septemba 28, 1979 na jina la Ndelikyama M. Mweleli, Kwa kusudi la kuonyesha kuwa Kiwanja namba 160 kilichopo Mbezi Beach Dar es Salaam, kilikuwa ni Cha Ndelikyama Mabolio Mweleli huku akijua wazi kuwa ni za uongo.