RAIS SAMIA MGENI RASMI MKUTANO WA UVUVI BARANI AFRIKA


Na lilian Ekonga 

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika  Mkutano wa Uvuvi barani Afrika (AFRICA SMALL SCALE FISHERIES SUMIT 2024) wenye lengo la kuimarisha umoja wa Afrika na kuwasilisha maoni ya Mkutano huo katika mikutano ya kimataifa kama Sauti Moja ya Afrika.


Hayo yalisemwa Jana na Waziri wa Mifumo na Uvuvi, Abdallah Ulega wakati akizungumza na waandishi wa Habari Jana Jijini Dar es Salaam kuhusu ujio wa mkutano huo ambao utafanyika Tarehe 5-7 Julai mwaka huu katika ukumbi wa mikutano Mlimani city Jijini Dar es Salaam 


"Pamoja na mambo mengine, mkutano huu utatumika kama Jukwaa litakolokutanisha wavuvi kutoka nchini Tanzania na wenzao kujadili mafanikio na changamoto zinazowakabili dhidi ya mustakabali wao."

Waziri Ulega alisema Mkutano huo utajumuisha maadhimisho ya miaka 10 ya utekelezaji wa Mwongozo wa Uvuvi Mdogo na Muundo wa kisera wa kusimamia Uvuvi na Ukuzaji Viumbe Maji barani Afrika, lakini pia utaangazia fursa zilizopo katika Uchumi wa Buluu.


"Mkutano huu utakuwa chachu ya kubadilishana mawazo, fursa na teknolojia mbalimbali za kuhakikisha nchi inapiga hatua kubwa kwenye utekelezaji wa dhana ya kujenga kesho iliyo bora kwa vijana wetu (BBT), na kufikia malengo makubwa kwenye Uchumi wa Buluu."

Aidha Waziri Ulega amesema mkutano huo unatarajia kujumuisha viongozi na wataalam wa sekta ya Uvuvi kutoka Afrika, Wawekezaji na Wafanyabiashara wakubwa barani Afrika na Ulimwenguni kwa ujumla, Taasisi zisizo za Kiserikali, Taasisi za Kikanda, Watafiti, Vyuo Vikuu, na Wavuvi Wadogo ambao ndiyo wahusika wakuu wa Mkutano huu.

Waziri Ulega aliyataja manufaa mbalimbali ambayo nchi itayapata kupitia Mkutano huu ikiwa ni pamoja na Kufungua fursa za uwekezaji kwenye sekta ya Uvuvi, Kufungua wigo wa masoko ya nje ya mazao ya Uvuvi ya nchini Tanzania, kuongeza uwanda mpana wa wavuvi nchini kujifunza namna ya kuendesha shughuli zao kisasa ili uvuvi wao uwe na tija, kuendelea kuboresha mahusiano ya matumizi ya rasilimali za maji ya asili na zile za ukuzaji viumbe maji, baina wa wadau  wa Sekta ya Uvuvi  waliopo hapa nchini na wale wa mataifa mengine barani Afrika na Ulimwenguni kwa ujumla.
Previous Post Next Post