TMA YATOA TAHADHARI KUBWA KUELEKEA MVUA ZA MASIKA 2024


Na Humphrey Msechu, Dar

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania TMA imetoa mwelekeo wa msimu wa mvua za Masika katika kipindi cha Machi hadi Mei 2024 ambazo zitakuwa za wastani hadi juu ya wastani nakutoa ushauri kwa wadau wa sekta hiyo.

Akizungumza na waandishi wa Habari Leo Jijini Dar es Salaam Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo Dkt. Ladislaus Chang’a amesema mvua hizo zinatarajiwa katika maeneo mengi ya nchi yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka.

“Ongezeko la mvua linatarajiwa katika kipindi cha mwezi Machi 2024 na mvua za Masika kuanza wiki ya nne ya mwezi Februari 2024 katika maeneo mengi na zinatarajiwa kuisha katika wiki ya tatu na ya nne ya mwezi Mei 2024 katika maeneo mengi “ Amesema Dkt. Chang’a.

Sambamba na hayo ametaja athari zinazoweza kujitokeza ikiwemo vipindi vya unyevu wa kuzidi kiasi na mafuriko vinaweza kujitokeza na kuathiri ukuaji wa mazao na miundombinu ya kilimo, kuongeza kwa kina cha maji katika mito na mabwawa na uwezekano wa kutokea magonjwa ya mlipuko sababu ya uchaguzi wa maji.

Amesema mvua za Masika ni mahsusi kwa maeneo ya nyanda za juu Kaskazini Mashariki ( mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro), Pwani ya Kaskazini ( Kaskazini mwa mkoa wa Morogoro, mikoa ya Pwani ikijunuisha visiwa vya Mafia, Dar es Salaam, Tanga pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba), ukanda wa ziwa Victoria (mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu na Mara pamoja na Kaskazini mwa mkoa wa Kigoma.

Hata hivyo amesema mifumo ya hali ya hewa joto la bahari la juu ya wastani linatarajiwa katika eneo la magharibi mwa bahari ya Hindi (Pwani ya Afrika Mashariki) ikilinganishwa na upande wa Mashariki mwa bahari ya Hindi huku joto la bahari la chini kidogo ya wastani linatarajiwa katika eneo ya kusini mwa kisiwa Cha Madagaska.

Wakulima wameshauriwa kuandaa mashamba , kupanda na kupalilia na kutumia pembejeo husika Kwa wakati, kutumia mbinu bora na teknolojia za kuzuia Maji kutuama shambani, mmomonyoko na upotevu wa rutuba na kuchagua mbegu na mazao sahihi Kwa ajili ya msimu huu wa Masika.

Hata hivyo ametoa wito kwa menejimenti za maafa kuwa vipindi vya mvua kubwa vinaweza kujitokeza na kusababisha mafuriko na maporomoko ya ardhi na kupelekea uharibifu wa miundombinu, mazingira, upotevu wa Mali na maisha hivyo Mamlaka husika ziendelee kuratibu utekelezaji wa mipango ya kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza.
Previous Post Next Post