UNICEF YAKABIDHI MISAADA WAATHIRIKI WA MAAFA HANANG’



NA. MWANDISHI WETU

Serikali imeendelea kupokea misaada mbalimbali kwaajili ya waathirika wa Maafa Hanang’ ambapo leo Disemba 08, 2023 Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto UNICEF limekabidhi misaada mbalimbali ya kibinadamu kwa lengo la kusaidia waathirika wa maafa Hanang’ huku wakisema wataendelea kushirikiana na Serikali.


UNICEF imewasilisha salamu zao za pole kwa waathirika wa Maafa Wilayani humo  kwa kutoa mahitaji mbalimbali vikiwemo nguo za Watoto, mablanketi, matanki ya kuhifadhia maji, ndoo za maji, sabuni, madawa na vifaa tiba, mitungi ya gesi na vitu vingine vyenye thamani ya Dola za Kimarekani elfu sitini na sita.


Aidha akipokea na kutoa neno la Shukran wakati wa makabidhiano hayo Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi amewashukuru kwa misaada na kuendelea kutoa wito kwa wadau zaidi kujitokeza.


“Tunawashukuru wadau wetu UNICEF, mmeonesha kututhamini na hii itatoa unafuu kwa waathirika na imeleta faraja kubwa kwetu, nasi tutasimamia vizuri kila vifaa na misaada inayoendelea kutolewa kwa kuratibu matumizi yake kama ilivyokusudiwa,” alisisitiza Dkt. Yonazi

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo Mwakilishi wa UNICEF Bw. Allan Rwechungura ametoa pole kwa waathirika wote wa maafa hayo, huku akisema Shirika litaendelea kutoa ushirikiano kwa Serikali.


Previous Post Next Post