TMA YATOA MWELEKEO MVUA ZA MSIMU MAENEO YANAYOPATA MSIMU MMOJA KWA MWAKA

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) Dkt. Ladislaus Chang'a akitoa mwelekeo wa mvua za Msimu (Novemba, 2023 – Aprili, 2024) kwa waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

Na Humphrey Msechu, Dar

MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imesema Mvua za Juu ya Wastani hadi Wastani zinatarajiwa katika maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka.

Hayo yamebainishwa leo Oktoba 31, 2023 na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA Dkt. Ladislaus Chang'a akitoa mwelekeo wa mvua za Msimu (Novemba, 2023 – Aprili, 2024) kwa waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

Dkt. Chang'a ametaja maeneo hayo kuwa ni ya kusini mwa Mkoa wa Morogoro, mikoa ya Iringa, Lindi, Mtwara, Singida, Dodoma, Kaskazini mwa Mkoa wa Katavi, Kigoma na Tabora.

"Aidha, mvua za Wastani hadi Juu ya Wastani zinatarajiwa kusini mwa mkoa wa Katavi, mikoa ya Njombe, Rukwa, Songwe, Mbeya na Ruvuma," amesema Dkt. Chang'a na kuongeza,

"Mvua zinatarajiwa kuanza wiki ya nne ya mwezi Oktoba, 2023 katika maeneo ya magharibi na kutawanyika katika maeneo mengine mwezi Novemba, 2023,".

Kwamba kipindi cha nusu ya kwanza ya msimu (Novemba, 2023–Januari, 2024) kinatarajiwa kuwa na mvua nyingi ikilinganishwa na nusu ya pili (Februari–Aprili, 2024) ambapo Uwepo wa El-Niño unatarajiwa kuwa na mchango mkubwa katika mvua za Msimu.

Kuhusu athari na ushauri Dkt. Chang'a ameeleza kuwa shughuli za kilimo zinatarajiwa kuendelea kama ilivyo kawaida katika maeneo mengi. 

Hata hivyo, ameeleza kwamba, vipindi vya unyevu wa kuzidi kiasi pamoja na mafuriko vinaweza kujitokeza na kuathiri ukuaji wa mazao na miundombinu ya kilimo na kusema kuwa kina cha maji katika mito na mabwawa kinatarajiwa kuongezeka. 

Hivyo Dkt. Chang'a amewashauri wadau mbalimbali kuzingatia matumizi endelevu na uhifadhi wa rasilimali maji.

Kuhusu Mwenendo wa Mvua za Vuli (Oktoba-Disemba), 2023, Dkt. Chang'a amesema Msimu wa Vuli kwa miezi ya Oktoba hadi Disemba, 2023 katika maeneo yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka (Mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Mara, Manyara, Arusha, Kilimanjaro, Tanga, Dar es Salaam, kaskazini mwa mkoa wa Morogoro, Pwani (ikijumuisha kisiwa cha Mafia) pamoja na Zanzibar (visiwa vya Unguja na Pemba)) utabiri wake ulitolewa Agosti 24, 2023. 

Kweamba Mvua za Juu ya Wastani hadi Wastani zilitarajiwa katika maeneo mengi ya pwani ya kaskazini na ukanda wa Ziwa Victoria. Aidha, kwa maeneo ya nyanda za juu kaskazini mashariki na maeneo machache ya mashariki mwa Ziwa Victoria mvua zilitarajiwa kuwa za Wastani hadi Juu ya Wastani. 

Dkt. Chang'a amebainisha kuwa Mvua hizo zimeshaanza katika maeneo ya ukanda wa Ziwa Victoria, pwani ya kaskazini na baadhi ya maeneo ya nyanda za juu kaskazini mashariki kama ilivyotabiriwa. 
Ameongeza kuwa, ongezeko la mvua linatarajiwa katika miezi ya Novemba na Disemba, 2023. Vilevile, mvua za nje ya msimu zinatarajiwa katika mwezi Januari na Februari, 2024.
Previous Post Next Post