Na Humphrey Msechi, Geita
WAKALA wa Majengo Tanzania (TBA) katika mwaka wa fedha 2023/2024 unatajia kujenga jengo la ghorofa la biashara na makazi katika Mkoa wa Geita.
Akijibu swali la Mbunge wa jimbo la Geita mjini Mhe. Constantine Kanyasu alipotembelea katika banda hilo katika maonesho ya sita ya teknolojia ya madini yanayaofanyika katika viwanja vya EPZA Bombambili Halmashauri ya Mji Geita ambapo mbunge huyo alitaka kujua endapo nje ya miradi ya ujenzi wa majengo ya ofisi za umma wakala huo una mpango wa kuwekeza miradi ya nyumba za makazi mjini Geita kama ilivyo katika mikoa mingine kama Dodoma.
Akijibu swali hilo
Kaimu Meneja Mawasiliano na Masoko - TBA, Fredrick Kalinga amesema kuwa TBA ina mpango wa kuanza ujenzi wa jengo la ghorofa ambapo chini litakuwa na kibiashara na kuanzia ghorofa ya kwanza kutakuwa na makazi.
"Mheshimiwa Mbunge katika bajeti ya mwaka huu tunatarajia kujenga jengo la ghorofa pale eneo la round about maarufu msikitini na taratibu zote zimekamilika na muda wowote tutaanza ujenzi wake "amesema Kalinga.
Aidha Kalinga ameongeza kuwa Serikali ya awamu ya sita imeona haja ya kuhuisha Sheria iliyoanzisha TBA kwa kuiboresha kupitia GN namba 595 ya tarehe 25 Agosti 2023 ambayo inairuhusu TBA kushirikiana na Sekta Binafsi kuendeleza miliki nchini kwa kujenga nyumba za kupangisha na kuuza kwa wananchi wote, hivyo kwa kushirikiana na Sekta Binafsi, TBA inatarajia kujenga nyumba nyingi za kuuza na kupangisha kwa wananchi wote.
Kwa kufanya hivyo itakua nafasi nzuri ya kuendeleza majengo mengi zaidi na tunatarajia taasisi itaongeza uwezo wake wa kutekeleza miradi mingi zaidi ya ujenzi wa nyumba za makazi.
Pia muda si mrefu Sekta Binafsi itaarifiwa namna gani watashirikiana na sisi TBA"ameongeza Kalinga
Kalinga ameongeza kuwa kuna miradi mbalimbali ambayo inatekelezwa na mingine tayari imeshakamilika kama hospital ya rufaa ya Kanda Chato, hospital ya rufaa ya mkoa na majengo ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita na wakuu wa Wilaya wa Mbogwe na Nyang’wale.
Kwa upande wake mbunge huyo wa Geita mjini amewapongeza TBA kwa kazi nzuri wanazozifanya na kuwakaribisha katika uwekezaji mbalimbali mjini humo.