WAZIRI DKT. MWIGULU AMEWATAKA VIONGOZI NCHINI KUTILIA MAANANI UMUHIMU WA TAKWIMU ZA SENSA ILIKUTEKELEZA MIRADI YA MAENDELEO


Na Mwandishi wetu

Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba,
amewataka viongozi nchini, kuhakikisha wanatilia maanani umuhimu wa takwimu zilizotokana na Sensa ya Watu na Makazi iliyofanyika Mwezi Agosti mwaka 2022, katika kupanga na kutekeleza miradi ya maendeleo, inayolingana na idadi ya watu waliopo kwenye eneo husika.

Mhe. Dkt. Nchemba, amesema hayo kwenye mafunzo kuhusu matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi, kutoka kwa wataalamu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, yaliyofanyika katika Wilaya ya Iramba, mkoani Singida.


Mafunzo hayo yalishirikisha wajumbe wa Kamati ya Sensa wa Halmashauri za Wilaya, manispaa na viongozi mbalimbali ngazi ya Kata, wilaya na Mkoa wa Singida.

Dkt. Nchemba alisema kuwa, ili huduma mbalimbali za kijamii ziweze kutosheleza katika jamii, ni muhimu kwa viongozi kutilia maanani umuhimu wa matokeo na maoteo (makadirio) ya sensa, ili miradi inayotekelezwa na
serikali iendane na mahitaji ya watu waliopo kwenye maeneo yao ikiwemo kukabiliana na upungufu wa huduma za jamii kamavile madarasa na madawati.

Awali, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, alitumia fursa hiyo kuipongeza Serikali ya Awamu ya Sita ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa uongozi wake uliotukuka katika kuliongoza Taifa, ambalo sasa limepiga hatua kubwa kimaendeleo.


Mapema Mkuu wa mkoa wa Singida, Bw. Peter Serukamba, akimkaribisha Waziri wa Fedha na Mipango kufungua mafunzo hayo, aliishukuru Ofisi ya Taifa ya Takwimu, kwa kujali na kuona umuhimu wa mafunzo hayo hadi ngazi ya chini, ili jamii iweze kuelewa na kuona umuhimu wa Takwimu kwa ajili ya maendeleo ya Taifa.

Aliwataka wananchi wa Iramba na Mkoa wa Singida kwa ujumla kuendelea kumuunga mkono waziri huyo, ambaye pia ni Mbunge wa Iramba Magharibi, katika maendeleo ya Taifa, na hasa anapomsaidia Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan, kwa ajili ya kuwaletea Watanzania wote, maendeleo ya kweli.
Previous Post Next Post