Tanesco yaanika mafanikio 2021/2022


Na Mwandishi Wetu, Dar

Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), limeweka wazi mafanikio yake ya mwaka 2021/2022, kutokana na ufanisi mkubwa wanaoufanya kupitia kwenye miradi yake ya kimkakati.

Yapo mafanikio mbalimbali walioyapata mwaka uliopita, kutokana na kuwa na timu bora yenye uwezo mkubwa ya kusimamia vipaumbele vyake.

Hayo yamesemwa leo na Mkurugenzi wa Tanesco, Maharage Chande katika kikao kazi kati ya Tanesco na msajili wa hazina na wahariri wa vyombo vya habari kwa ajili ya kuelezea mafanikio na kazi za shirika hilo.

Chande amesema, vupaumbele ambavyo vimelifanya Shirika hilo kupiga hatua ni, ufanisi katika nyanja mbalimbali, kuwa na miradi ya kimkakati, mawasiliano na ushirikishaji wa wadau.

Vipaumbele vingine ni kuwa na wateja, Rasilimali fedha pamoja na udhibiti wa utawala ambapo kila mfanyakazi katika shirika hilo anajua wajibu wake.

Hata hivyo, Mkurugenzin huyo amesema mafanikio makubwa waliopata katika vupaumbele vyao ni mradi wa Bwawa la kuzalisha umeme la Julius Nyerere (JNHPP) ambao umefikia asilimia 90 kumalizika.

Licha ya gaharama za uzalishaji wa umeme kutarajiwa kushuka baada ya kukamilika kwa Bwawa hilo Juni 2024, imebainika kuwa uzalishaji huo hautapunguza bei ya umeme kwa wateja.

Bwawa hilo linatarajia kuzalisha megawati 2,115 za umeme zitakazoingizwa katika Gridi ya Taifa.

Aidha, Chande amesema mwaka 2020/2021 gharama ya uzalishaji wa umeme ulikuwa Sh1.5 trilioni ikilinganishwa na ongezeko la Sh 1.6 trilioni kwa mwaka 2021/2022.

“Mradi wa Mwalimu Nyerere ukikamilika gharama za umeme zitashuka lakini hatutashusha bei kwasababu tutashindwa kupiga hatua,” amesema.

Chande alitoa mchanganuo wa matumizi ya umeme kwamba mpaka sasa shirika hilo linawateja milioni 4.4, ambao miongoni mwao wateja wa viwandani ni 4,000 na majumbani zaidi ya milioni tatu.

Kiwango hicho kinawafanya wananchi kutumia asilimia 50 ya megawati 1400 zinazozalishwa na Tanesco kila siku na viwanda nako ni asilimia 50.

Naye Makamu Mkurugenzi wa uzalishaji umeme Tanesco, Pakaya Mtamakaya amesema mwaka 2020/2021 upotevu ulikuwa wa asilimia tisa lakini kufikia 2021/2022 upotevu ukipungua kufikia asilimia 8.

Amesema, sababu ya upotevu wa umeme ni umeme wenye kilovoti ndogo kusafirishwa umbali mrefu na sasa wanaendelea na mkakati wa kupunguza upotevu.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Huduma kwa wateja wa Tanesco, Martin Mwambene amesema moja ya kipaumbele cha shirika hilo ni wateja kwani ni Kurugenzi ya kwanza kuanzishwa tokea shirika hilo lianzishwe.

Mwambene amesema, Tanesco imeanzisha huduni ya Nikonekti ambayo inamrahisishia mteja kuomba umeme akiwa nyumbani kwake.

“Mafanikio ya huduma hii yamepiga hatua kwani tumeweza kuwaungashia umeme wateja zetu kwa mwaka mmoja takribani 500,400,” amesema Mwambene.
Previous Post Next Post