TEA - KUTUMIA SH BILIONI 8.9 KUFADHILI MIRADI YA KUBORESHA MIUNDOMBINU YA ELIMU NCHINI.



Katika mwaka wa fedha wa 2022/2023 Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) imepanga kutumia kiasi cha Sh. Bilioni 8.9 kwa ajili ya kufadhili miradi ya kuboresha miundombinu ya elimu nchini

Kiasi hicho cha fedha kitatumika kufadhili wa miradi 96 katika shule 96 za msingi na sekondari katika maeneo mbali mbali ya Tanzania Bara pamoja na Taasisi mbili za elimu ya juu kwa upande wa Tanzania Zanzibar.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Agosti 4,2022 Jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) Bi. Bahati I. Geuzye amesema Miradi itakayofadhiliwa ni pamoja na Ujenzi wa madarasa 99, matundu ya vyoo 792, maabara kumi za masomo ya sayansi kwa ajili ya shule 05 za sekondari, nyumba za walimu 52 na Mabweni 10.

Amesema miradi mingine itakayotekelezwa ni ujenzi wa miundombinu ya wanafunzi wenye mahitaji maalum inayojumuisha madarasa 10, matundu ya vyoo 40 pamoja na mabweni mawili katika shule 6 za msingi na moja ya sekondari.

Bi.Geuzye amesema katika mwaka huu wa fedha 2022/23 Mfuko wa Elimu wa Taifa utaboresha miundombinu na kuwezesha ununuzi wa vifaa vya kujifunzia na kufundishia kwa taasisi mbili za elimu ya juu zilizopo Tanzania - Zanzibar. Miradi hiyo imepangwa kutumia Shilingi Milioni 500 katika utekelezaji wake.


Amesema Mamlaka imewezesha utekelezaji wa miradi 3,314 yenye thamani ya shilingi bilioni 212.6 ambapo taasisi za elimu zikiwemo shule za awali, shule za msingi, shule za sekondari, vyuo vya ualimu, vyuo vya ufundi na vyuo vikuu vimenufaika.

Aidha amesema katika mwaka wa fedha wa 2021/2022, TEA ilipokea michango na kutekeleza miradi ya pamoja na mashirika ya Umma na yasiyo ya kiserikali yenye thamani ya Shilingi Milioni 556.3.

"Mashirika hayo yaliyoshirikiana na TEA ni pamoja na Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), Taasisi ya Flaviana Matata, BRAC- Maendeleo Tanzania, Taasisi ya Asilia Giving, Taasisi ya SAMAKIBA na Kampuni ya Dash Industries". Amesema Bi.Geuzye.

Pamoja na hayo amesema kupitia Mfuko wa Elimu wa Taifa unaoratibiwa na TEA, katika mwaka wa fedha 2021/2022, Shilingi bilioni 8.6 ziligharimia ufadhili wa miradi 160 ya kuboresha miundombinu ya elimu katika shule 151 nchini.

"Miradi hiyo ilijumuisha ujenzi wa madarasa 210 katika shule 65 (za msingi 53 na sekondari 22), Maabara 4 za sayansi katika Shule 2 za Sekondari, Matundu ya vyoo 1920 katika shule 80 (za msingi 58 na sekondari 22), vifaa vya kujifunzia na kufundishia katika shule 09 za wanafunzi wenye mahitaji maalum(shule 08 za msingi na moja ya sekondari) na ujenzi wa ofisi mbili za walimu katika shule mbili za sekondari". Amesema


Hata hivyo amesema kuwa katika awamu ya kwanza ya utekelezaji wa miradi yakuratibu Mfuko wa Kuendeleza Ujuzi (Skills Development Fund-SDF), mafunzo yalijikita katika sekta ya Kilimo na Kilimo - Biashara, shilingi bilioni 3.1 zilitumika kufadhili taasisi 15 za kutoa mafunzo ya ujuzi.


Ameeleza kuwa kupitia mfuko huo kiasi cha Shilingi Milioni 385.8 kimetolewa kunufaisha vijana 1,018 katika programu ya Utarajari (Internship Program) katika sekta za TEHAMA, Utalii na huduma za ukarimu; Nishati; Ujenzi na Uchukuzi.


Amesema Mfuko wa SDF pia unafadhili mafunzo ya Ujuzi kwa wanufaika 4,000 kutoka Kaya Maskini na Makundi Maalum (Bursary Scheme) hadi ifikapo Desemba 2022 lengo ni kuwezesha vijana wanaotoka katika kaya maskini kupata ujuzi na kujikwamua kiuchumi.

Previous Post Next Post