WANANCHI WILAYANI MPWAPWA WAMEPEWA RAI KUENDELEZA MIRADI YA MAENDELEO ILIYOTEKELEZWA

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) Dkt. Switbert Mkama akipata maelezo kutoka kwa Bw. Peter Kadala Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Peen Construction Ltd wanaohusika na uchimbaji wa lambo katika Kijiji cha Kazania, Wilayani Mpwapwa. Lambo hilo pia litanufaisha na Kijiji Jirani cha Kiegea



Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) Dkt. Switbert Mkama akikagua ukamilikaji wa kisima kimojawapo kwa kuangalia wingi wa maji katika Kijiji cha Mbugani, Wilayani Mpwapwa ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi kwa kutumia mifumo Ikolojia unasimamiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais.



Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) Dkt. Switbert Mkama akipata maelezo kuhusu Mashine ya kukamua alizeti na kukagua ubora wa mafuta hayo katika Kijiji cha Ng’hambi chini ya Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi kwa kutumia mifumo Ikolojia unasimamiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais, ziara hiyo imefanyika leo 02/08/2022



                 Na Mwandishi Wetu

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) Dkt. Switbert Mkama ametoa rai kwa wakazi wa Wilaya ya Mpwapwa kusimamia kikamilifu miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo yao.
 
Ametoa rai hiyo leo Agosti 2, 2022 akiwa katika ziara ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi kwa kutumia mifumo Ikolojia (Ecosystem-Based Adaptation for Rural Resilience in Tanzania - EBBAR) unaotekelezwa Wilayani Mpwapwa.
 
Dkt. Mkama ameshuhudia kukamilika kwa visima virefu vinne vyenye uwezo wa kutoa lita elfu 40,000 kwa siku ambavyo vinanufaisha wakazi wa Vijiji vya Nghambi, Mbugani, Kiegea na Kazania.
 
"Serikali inatafuta fedha za kutekeleza miradi hii yenye faida kubwa kwa wananchi, natoa rai kwenu muitunze, iwasaidie na kuleta manufaa sasa na kwa vizazi vijavyo" Alisisitiza Dkt. Mkama.
 
Pia, amewataka wanufaika wa miradi hiyo kuongeza kasi ya upandaji miti katika maeneo yao na kujishughulisha na kilimo rafiki kwa mazingira kama chanzo mbadala cha kujiongezea kipato na kutolea mfano wa kilimo cha Mboga mboga.
 
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Ng’hambi Bw. Richard Milimo amesema Mradi wa Ebbar umekuwa ni mkombozi kwa wakazi wa Mpwapwa kwa kuwa umetatua changamoto ya maji iliyokuwa ikiwakabili kwa muda mrefu.
 
Kiasi cha Shilingi Milioni Mia nane zimetumika Wilayani Mpwapwa kupitia Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi kwa kutumia Mifumo Ikojia ambapo mipango ya matumizi ya ardhi imeandaliwa, visima virefu vinne, Malambo mawili, Majosho mawili, vitalu nyumba vitatu na mashine ya kukamulia alizeti vimepatikana kupitia utekelezaji wa mradi huo unaosimamiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais.

Mradi huu pia unatekelezwa katika Halmashauri za Kaskazini A (Unguja), Simanjiro (Manyara), Mvomero (Morogoro) na Kishapu (Shinyanga).
Previous Post Next Post