MKANDARASI APEWA SIKU 14 KUKAMILISHA UJENZI TANKI LA MAJI WILAYA YA MVUMERO

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) Dkt. Switbert Mkama akipata maelezo kutoka kwa Bw. Erasto Nyahila Mwakilishi wa Kampuni ya Babenko inayohusika na uchimbaji wa visima na ujenzi wa mnara wa tanki la maji litakalotumika kutoa huduma ya maji kwa wakazi wapatao 1250 katika Kijiji cha Mingo, Wilaya ya Mvomero Mkoani Morogoro kupitia Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi kwa kutumia mifumo Ikolojia Vijiijini – EBARR unaosimamiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais.


Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) Dkt. Switbert Mkama akikagua ujenzi wa mnara wa tangi la maji katika Kijiji cha Mingo, Wilayani Mvomero ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi kwa kutumia mifumo Ikolojia unasimamiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais.


         Na Mwandishi Wetu

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) Dkt. Switbert Mkama ametoa muda wa siku 14 kwa Mkandarasi wa Kampuni ya Dabenko Enterprises Ltd kukamilisha ujenzi wa tanki la maji litakalotumika kutoa huduma ya maji kwa wakazi wapatao 1250 katika Kijiji cha Mingo, Wilaya ya Mvomero Mkoani Morogoro.

Ametoa rai hiyo leo Agosti 2, 2022 akiwa katika ziara ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi kwa kutumia mifumo Ikolojia Vijiijini – EBARR unaotekelezwa Wilayani Mvomero. Dkt. Mkama amemtaka Mkandarasi huyo kukamilisha haraka na kwa viwango vinavyokubalika ujenzi wa mnara wa tanki la maji na kurekebisha kasoro zilizoonekana.

"Hakikisha ujenzi huu unakamilka kama ilivyoelekezwa kwa mujibu wa mkataba na maboresho yafanyike katika maeneo ya umaliziaji na dirisha hili litolewe, liwekwe lenye viwango" Alisisitiza Dkt. Mkama.

Ametoa rai kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mvomero kusimamia miradi hiyo ili thamani ya fedha ilingane na ubora wa kazi za mradi wenyewe.

Nae Mwakilishi wa Kampuni ya Babenko inayohusika na ujenzi wa tanki hilo Bw. Erasto Nyahila ameahidi kurekebisha kasoro zote zilizobainika ndani ya muda uliopangwa.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kijiji cha Mingo Bw. Rashid Athumani amesema kukamilika kwa uchimbaji na ujenzi wa kisima chenye urefu mita 150 katika Kijiji chao utasaidia shughuli za kilimo cha umwagiliaji mwaka mzima na matumizi ya nyumbani.

Bilioni 1.16 zimepelekwa katika Wilaya ya Mvomero kwa ajili ya ujenzi wa skimu ya umwagiliaji, uchimbaji wa visima vinne, malambo mawili, majosho mawili na kiwanda kidogo cha kuzalisha sabuni, kiwanda kidogo cha bidhaa za Ngozi, na kituo cha kukusanyia maziwa.

Shughuli nyingine zinazotekelezwa na Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi kwa kutumia Mifumo Ikojia vijiijini kwa Wilaya ya Mvomero ni pamoja na ujenzi wa vitalu nyumba kwa ajili ya kilimo cha mbogamboga na majiko banifu kwa kaya 516.
Previous Post Next Post