NEVILE Meena, Mjumbe wa Kamati Utendaji ya Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), amesema miongoni mwa sababu za kupendekeza wanahabari wenye taaluma nyingine kubaki katika vyumba vya habari, ni kupata mchanganyiko wa taaluma kwenye habari.
Neville Meena, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), ametoa kauli hiyo wakati akizungumza katika kipindi cha Pambazuko kinachorushwa na MVIWATA FM, mjini Morogoro
Amesema, wapo wanahabari ambao hawakupita kwenye vyuo vya uanahabari lakini kutokana na kukaa kwao kwenye vyumba vya habari, walikuwa wanahabari wazuri.
“Wapo walioingia kwenye vyumba vya habari wakiwa wa Shahada ya taaluma nyingine akiwemo Mwenyiti Mstaafu wa TEF, Absalom Kibanda na wamefanya vizuri kwenye taaluma ya habari,” amesema Meena.
“Lakini sheria hii pia tumependekeza waandishi wapya wanaoingia kwenye taaluma ya habari, lazima wawe na kiwango cha elimu angalau diploma,” amesema Meena.
Akizungumzia mchakato wa mabadiliko ya sheria ya habari, Meena amesema, serikali iliona kuna kila sababu ya kushughulika na sheria za habari na ndio maana yenyewe ilianza kupendekeza mabadiliko na kutuletea sisi.
“Baada ya malalamiko ya wadau wa habari, serikali ya awamu hii (Awamu ya Sita) ilisikia na ndio iliyoanza kuleta mapendekezo ya mabadiliko ya sheria. Kwenye mapendekezo hayo, ilianza katika kipengele cha 38.
“Sasa mapendekezo hayo yalipotufikia sisi wadau wa habari, tulikaa kwa pamoja na tukasema tuanze na kipengele cha kwanza. Na kwa kuwa ilikuwa na dhamira ya kweli ya kupitia mabadiliko ya vipengele hivyo, tayari kikao cha kwanza cha wadau na serikali kimeishafanyika,” amesema.
Katika kipindi hicho Meena amesema, Serikali ilianza kuonesha dhamira ya dhati tangu pale Rais Samia Suluhu Hassan alipokaa kikao na wanahabari Ikulu, Dar es Salaam.
“Si hivyo tu, bado Rais Samia aliagiza kufunguliwa kwa televisheni za mtandao iliyokuwa zimefungiwa, na zaidi katika Serikali yake hiyo hiyo magazeti yaliyokuwa yamefungwa kipindi kirefu nayo yalifunguliwa.
“Yote haya yanaonesha kwamba, suala la Serikali kutaka kumaliza malalamiko ya wadau wa habari nchini lipo wazi, na sisi tunatumia wakati huu kuhakikisha tunafikia malengo,” amesema Meena.