Na John Mapepele
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe, Mohamed Mchengerwa amesema huu ni wakati wa kuongeza ubunifu kwenye utendaji kwa tasnia ya utoaji wa huduma katika sherehe ili kutoa ajira na kuongeza vipato vyao kwa ujumla.
Mhe. Mchengerwa ametoa wito huo leo Mei 15, 2022 kwenye Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam wakati akitoa hotuba yake kwenye kilele cha maonesho ya tano ya biashara yanayowajumuisha watoa huduma wote kwenye sherehe baada ya kukagua mabanda yote ya washiriki.
Watoa huduma hao ni pamoja na washereheshaji, wauzaji wa nguo za harusi, wapishi, wapiga picha wenye saloon na watengenezaji keki.
Aidha, amewaomba watumie mashirikisho yao ili iwe rahisi kwa Serikali kutatua changamoto zinaziwakabili.
Kuhusu Serikali kutoa mikopo kwa watoa huduma amesema tayari Rais Samia Suluhu Hassan ameshatoa 1.5 bilioni kwa ajili yao na kuwaomba kuwasilisha maandiko Serikalini kupitia mashirikisho yao ili waweze kupata mikopo hiyo bila riba yoyote.
Aidha, kuhusu kuwa na kumbi kwa ajili ya watoa huduma amefafanua kuwa Serikali inadhamiria kujenga ukumbi wa Sanaa na Maonesho jijini Dar es Salaam ambao utachukua takribani watu 20000 kwa mara moja.
Amewataka wanatasnia ya utoaji wa huduma kuendeleza umoja baina yao kwa madai kuwa sekta hizo za Utamaduni, Sanaa na Michezo ni nguvu shawishi ya Serikali inayosaidia kuleta amani, mshikamano na furaha kwa wananchi ambapo amewasihi kumwombea Rais Samia ili aendelee kuiongoza vema Serikali yake kwa manufaa ya wananchi wake.
Katika tukio hilo Mhe, Mchengerwa ametoa vyeti kwa washiriki wote wa onesho hilo na kukata keki ya miaka mitano ya taasisi ya maonesho ya "Adorable Wedding Trade" kwa kutimiza miaka mitano tangu kuanzishwa kwake.
Pia Mhe. Mchengerwa amechezesha droo kwa ajili ya kuwapata wachumba wanaotarajia kufunga ndoa watakaogharimiwa kwa asilimia 80 na taasisi hiyo ambapo Isaac Miraji Msofe
na Diana Tangira wameibuka washindi.
Amesema Serikali itaendelea kuwajali kwa kuwa shughuli za sherehe zinatoa ajira kwa watu wengi hapa nchini.
Mtendaji Mkuu wa Adorable Wedding Trade Anna Lema amemshukuru na kumpongeza Mhe. Mchengerwa kwa kusimamia vizuri sekta anazoziongoza.
Aidha, maonesho mbalimbali ya wadau wa watoa huduma hao yamepamba tukio hilo.