Halmashauri zote za mkoa wa Dar es Salaam zimetakiwa kuweka mikakati ya kuwatumia wahudumu wa Afya ngazi ya jamii kuwaibua wasichana na akina mama wenye matatizo ya fistula ili waweze kupatiwa matibabu.
Kauli hiyo imetolewa leo Mei 20,2022 jijini Dar es Salaam katika kuadhimisha siku ya kimataifa ya kutokomeza fistula.
Akizungumza kwa niaba ya mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam , Mganga mkuu wa mkoa huu Dkt.Rashid Mfaume amesema hakuna haja ya wanawake wanaosumbuliwa na Fistula kujificha na badala yake wajitokeze na kufika katika hospitali ya CCBRT ambapo matibabu ya fistula yanapatikana bila malipo ikiwa ni pamoja na nauli.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji mkuu wa CCBRT Brenda Msangi amesema tangu kuanza kwa mapambano ya fistula mwaka 2003 wamepiga hatua kubwa Kitaifa katika kutoa matibabu ya Fistula kwa maelfu ya akina mama wenye tatizo hilo ambapo zaidi ya akina mama 17,500 wamepatiwa matibabu CCBRT na katika hospitali washirika.
Nao baadhi ya wagonjwa wa fistula wanaotibiwa katika hospitali CCBRT wametumia nafasi hiyo kuwataka akina mama walioathirika na ugonjwa huo kutojitomeza na kupatiwa matibabu kwani ugonjwa wa Fistula unatibika.
Tarehe 23 Mei ya Kila mwaka Tanzania huungana na nchi nyingine duniani kuadhimisha siku ya Kimataifa ya kutokomeza Fistula ya uzazi ambapo kwa hapa nchini yatafanyika mkoani Mwanza huku yakibeba kauli mbiu isemayo " Tokomeza fistula,Wekeza,imarisha huduma za Afya na wezesha jamii".