TUME YA MADINI YAENDELEA KUBUNI MIKAKATI YA UKUSANYAJI WA MADUHULI





Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba amesema kuwa Tume ya Madini imeendelea kubuni mikakati mbalimbali ya kuhakikisha inavuka lengo ililopewa la kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 650 kwa mwaka wa fedha 2021-2022 ifikapo Juni mwaka huu ikiwa ni pamoja na kuimarisha usimamizi kwenye shughuli za uchimbaji na biashara ya madini na kuongeza vitendea kazi.

Mhandisi Samamba aliyasema hayo leo kwenye ziara ya Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Msafiri Mbibo kwenye Ofisi za Tume ya Madini Makao Makuu jijini Dodoma ambapo alikutana na viongozi wa Tume kwa lengo la kujifunza majukumu ya Tume na kutatua changamoto mbalimbali.


Alisema kuwa katika kuimarisha Sekta ya Madini nchini hadi kufikia tarehe 23 Februari, 2022 jumla.ya magari saba yalipokelewa na kuongeza kuwa magari mengine 33 yapo njiani ikiwa ni kama mkakati wa kuhakikisha Tume inapata vitendea kazi vya kutosha katika kusimamia Sekta ya Madini.

Alieleza mikakati mingine kuwa ni pamoja na kusogeza huduma karibu na wananchi ikiwa ni pamoja na uanzishwaji wa Ofisi za Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa 29, Ofisi za Maafisa Migodi Wakazi 13 pamoja na Maabara moja ya kufanya tathmini ya sampuli za madini, kuchambua na kuthaminisha madini yanayozalishwa iliyopo jijini Dar es salaam.



Aliongeza mikakati mingine kuwa ni pamoja na uanzishwaji wa masoko 42 na vituo vidogo vya ununuzi wa madini 70 nchini, kati ya masoko hayo 27 ni ya madini ya dhahabu, masoko 14 ya madini ya vito na soko moja la madini ya bati.

Katika hatua nyingine akielezea hali ya ukusanyaji wa maduhuli kwa Mwaka wa Fedha 2021-2022, Mhandisi Samamba alisema kuwa kuanzia kipindi cha mwezi Julai 2021 hadi Februari, 2022 Tume imefanikiwa kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 412.27 sawa na asilimia 63.4 ya lengo la mwaka husika.


Alisema pia mchango wa Sekta ya Madini kwenye Pato la Taifa mwaka 2020 ulikua hadi kufikia asilimia 6.7 kutoka asilimia 4.8 mwaka 2018.

#sparklight_tvupdates #sparklight_tvupdates
Previous Post Next Post