Times FM na THT Wampa Tano Rais Samia



Kituo Cha Redio Cha Times Fm kilichopo Kawe Beach Dar es Salaam  kwa kushirikiana na Taasisi ya Tanzania House of Talent (THT) leo Machi 28, 2022 wameadhimisha kilele cha wiki ya Rais Samia ikiwa ni kampeni yenye nia ya kuuelimisha umma kuhusu mafanikio ya mwaka mmoja wa utendaji wake  tangu alipoanza majukumu yake kama Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Machi 19, mwaka 2021.

Mgeni Rasmi katika hafla hiyo ni Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Hassan Abbasi, ambaye amemuwakilisha Waziri Mhe. Mohamed Mchengerwa.


Akizungunza katika hafla hiyo Dkt. Abbasi ameleza mafanikio ya Rais Samia ndani ya mwaka mmoja kwenye sekta za utamaduni, sanaa na michezo ikiwemo Kuanzisha upya Mfuko wa Maendeleo ya Utamaduni na Sanaa, kuanzisha Tuzo za filamu na muziki, kuongezeka makusanyo na kutolewa kwa mirabaha, kuratibu mashindano ya urembo na mitindo kwa viziwi Afrika.


Ameyataja Mafanikio mengine kuwa ni kuanzishwa Mfuko wa maendeleo ya michezo na kutengewa asilimia 5 ya fedha za kubashiri matokeo ya michezo, ujenzi wa miundombinu ya kisasa ya michezo ikiwemo kumbi kubwa kwa ajili ya michezo na Sanaa za ndani (Sports and Arts Arena) utakaokuwa na uwezo wa kuchukua mashabiki 15,000 na kujengwa katika mikoa ya Dar es Salaam na Dodoma ambapo hatua za kuanza ujenzi wa miradi hii zinaendelea.

Taasisi ya Vipaji (THT),wamepamba tukio hilo  Kwa kuimba nyimbo nzuri maalum kwa ajili ya Rais Samia kama vile Ahadi, 100 za Samia na Karibu Tanzania inayoelezea vivutio mbalimbali vilivyopo nchini.
Previous Post Next Post